Friday, June 3, 2011

MWONGOZO WA KUANZISHA KLABU ZA WAPINGA RUSHWA KATIKA VYUO NCHINI



1.  UTANGULIZI
Mapambano  dhidi  ya  rushwa  si  ya  Serikali  au  Taasisi  ya  Kuzuia  na  Kupambana  na
Rushwa  peke  yake  bali  ni  ya  jamii  nzima.  TAKUKURU  ina  jukumu  la  kuongoza  na
kushirikisha  jamii  nzima  katika  mapambano  haya.  TAKUKURU  kupitia  Idara  ya  Elimu
kwa  Umma  hutumia  mbinu  mbalimbali  kuwaelimisha  na  kuwashirikisha  wanajamii  wa
makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na vijana walioko vyuoni katika  mapambano dhidi
ya rushwa.
Vijana ni rasilimali ya taifa,  watendaji wa sasa na siku zijazo na   chachu ya mabadiliko
katika  jamii.  Umuhimu  wa  vijana  ni  wa  kipekee  katika  kuleta  mabadiliko  ya  kijamii
hususani  katika  kubadili  mtazamo  mzima  wa  rushwa  kwa  jamii  ya  kitanzania  kutoka
kwenye  mtazamo  kuwa  rushwa  ni  sehemu  ya  utamaduni  na  kuiona  rushwa  kuwa  ni
tatizo la kitaifa lisilotakiwa kuvumiliwa kwa namna yoyote. Ili rasilimali hii iweze kutumika
vizuri zaidi, kuna umuhimu wa kuhamasisha uanzishwaji wa klabu hizi katika vyuo vya
elimu nchini.
TAKUKURU inatarajia kuzishirikisha klabu hizi katika mapambano dhidi ya rushwa kwa
namna mbalimbali  ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha wanachama wa klabu hizi  kwa njia
ya semina, matamasha ya sanaa, midahalo, kuwashirikisha  wanachama wa  klabu hizi
na walezi wao katika maadhimisho tunayoandaa na kushiriki  na kuwashirikisha kwenye
vipindi vya redio na televisheni.
Aidha,  ili  kuwafikia  na  kuwaelimisha  walengwa  TAKUKURU  itashirikiana  na  wadau
wengine wa mapambano dhidi ya rushwa ambao ni pamoja na Taasisi za dini, mashirika
ya umma, mashirika yasiyo ya kiserikali, asasi za kiraia na sekta binafsi.
1


2.  LENGO LA KUANZISHA KLABU
Klabu za wapinga rushwa katika vyuo zinaanzishwa kwa lengo la kuwajenga wanachuo
kimaadili na kuwashirikisha katika mapambano dhidi ya rushwa  kwa :-
a)  Kuwawezesha  vijana kutambua  nafasi  na  wajibu wao katika  mapambano dhidi
ya rushwa na hivyo kushiriki ipasavyo katika kuzuia na kupambana na rushwa.
b)  Kuwajenga  vijana  kimaadili  kwa  kuwafanya  watambue  madhara  ya  rushwa  ili
waichukie katika maisha yao na kuchukua hatua za kuzuia na kupambana nayo
hatimaye kujenga jamii ya watu waadilifu.
c)  Kuiwezesha  jamii  kutambua  nafasi  na  wajibu  wao  katika  mapambano  dhidi  ya
rushwa.
3.  UTAR ATIBU WA KUANZISHA KLABU
1)  Wanach uo  wenye  nia  ya  kuanzisha  klabu  wajikusanye  na  kuhamasisha
wanachuo wenzao umuhimu wa kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa.
2)  Wanachuo wachague wawakilishi  watakaowasiliana na TAKUKURU kwa ajili ya
kupewa semina kuhusu rushwa na kuzindua klabu husika.
3)  Katika kila chuo kuwe na klabu moja tu hata kama idadi ya wanachama itakuwa
kubwa.
4)  Mkuu wa chuo ateue mwalimu mlezi wa klabu ambaye ni mwadilifu.
5)  Mwalimu mlezi aitishe kikao kwa ajili ya kuchagua viongozi wa klabu kwa njia ya
demokrasia. Viongozi hao ni mwenyekiti, makamu mwenyekiti na katibu.
6)  Shughuli zote zinazofanywa na klabu zisikiuke sheria, kanuni na taratibu za nchi
na zifahamike kwa uongozi wa chuo na TAKUKURU.
7)  Taarifa za utendaji wa  klabu zitolewe kwa TAKUKURU  kupitia kwa uongozi  wa
chuo kisha kuwasilishwa Makao Makuu.
8)  Klabu iwe na katiba itakayoonyesha sifa  za mwanachama, malengo, taratibu za
uchaguzi  wa  viongozi,  idadi  ya  wanachama,  ukomo  wa  uanachama.  Aidha,
katiba iwasilishwe ofisi za TAKUKURU  ili kuhakikiwa  na baadae ithibitishwe na
kusainiwa  na  Mkuu  wa Chuo. Katiba  itawaongoza  katika  kutekeleza  majukumu
ya klabu.
2


4.  SIFA ZA MWANACHAMA
1.  Awe mwanachuo  wa chuo husika
2.  Awe mwadilifu
3.  Awe  tayari    kushiriki  katika  mapambano  dhidi  ya  rushwa  kwa  kutoa  taarifa,
kutojihusisha na vitendo vya rushwa, kukemea vitendo vya rushwa na kuelimisha
wanafunzi wenzake na jamii kwa ujumla
4.  Atii  sheria, kanuni na taratibu za chuo na nchi
5.  Awe na moyo wa kujituma, kujitolea na kushirikiana na wenzake.
6.  Ukomo  wa  uanachama  kwa wanachama wa  klabu  za wapinga  rushwa ni  pale
mwanachuo  anapohitimu  masomo,  anapojitoa  mwenyewe  au  kutolewa  kwa
sababu ya utovu wa nidhamu.
7.  Ukomo  wa  mwanafunzi kujiunga  na  klabu  ni  mwaka  mmoja  kabla  ya  kuhitimu
masomo.
5.  SIFA ZA KIONGOZI
1.  Awe mwanachama wa klabu kwa muda usiopungua miezi 6.
2.  Awe anashiriki katika shughuli zote za klabu.
3.  Awe na uwezo wa kujieleza, ujasiri, uwazi na ukweli.
4.  Awe mwepesi wa kusikiliza na kutoa maamuzi katika masuala yote ya klabu.
5.  Uchaguzi ufanyike mara moja kila mwaka.
6.  Nafasi za uongozi ziwe 3 tu ( mwenyekiti, makamu mwenyekiti na katibu).
7.  Asiwe mwanachama aliye katika mwaka wa mwisho wa masomo.
6.  MIKUTANO
1.
Mikutano  ya  kujadili  maendeleo  na  masuala  mbalimbali  ya  klabu  ifanyike
kulingana na utaratibu mtakaojiwekea kwa kufuata ratiba za masomo.
2.
Iwapo kuna dharura viongozi wa klabu wanaweza kuitisha kikao cha dharura kwa
kutoa taarifa ya muda mfupi kwa wanachama.
7.  SHUGHULI ZA KUFANYA
1)  Kujielimisha na kujua haki za raia.
3


2)  Kuelimisha  wanachuo  wenzao na jamii  kwa  ujumla  kuhusu  maana  ya  rushwa,
sababu za kuwepo kwa rushwa, madhara ya rushwa na umuhimu wa kuzuia na
kupambana na  rushwa.
3)  Kufanya midahalo  ndani na nje ya chuo kuhusu rushwa.
4)  Kufanya mijadala  ya  wazi itakayoibua  hoja na  changamoto  mbalimbali  kuhusu
mapambano dhidi ya rushwa.
5)  Kufanya maonyesho ya  sanaa  yenye ujumbe wa  mapambano dhidi ya  rushwa
kwa njia ya nyimbo, maigizo, ngonjera na nyinginezo.
6)  Kushiriki katika shughuli za kijamii.
7)  Kushiriki  kuandika  insha,  makala,  kuchora  katuni  na  hadithi  mbalimbali  zenye
maudhui ya kuelimisha na kukemea rushwa.
8)  Kutoa taarifa za vitendo vya rushwa TAKUKURU.
9)  Kushiriki  katika  maonesho,  matamasha  na  makongamano  mbalimbali
yatakayoandaliwa na TAKUKURU au Asasi nyingine kwa ajili ya kueneza ujumbe
wa kushirikisha jamii kupambana na rushwa.
10) Kujifunza utendaji  kazi katika sekta ya umma na binafsi kwa kuwaalika viongozi
wa sekta kuongea nao wakati wa vikao vyao kwa  lengo la  kupanua uelewa wa
haki na wajibu wao katika huduma mbalimbali zitolewazo kwa wananchi.
11) Kushirikiana na Kamati  za  Uadilifu  zilizoanzishwa katika halmashauri zenu  kwa
kutoa taarifa za ukiukwaji wa maadili.
12) Kushirikiana na  Kamati za Uadilifu zilizoanzishwa vyuoni kujenga maadili katika
vyuo.
8.  HITIMISHO
Ni  wazi  kuwa  vijana  ni hazina  muhimu  ya  taifa.  Umuhimu  wao  katika  jamii  yoyote  ni
chachu  pekee  ya  kuleta  mabadiliko  ya  kijamii,  kisiasa,  kiuchumi  na  kimaendeleo,  ili
kujenga  kizazi  kisichovumilia  wala  kukumbatia  rushwa  katika  kutekeleza  majukumu
yake.
Mafanikio  ya  mapambano  dhidi  ya  rushwa  yanategemea  kijana  kwani  kukataa
kwako rushwa kuna thamani. Aidha, uadilifu wako na wangu utaitokomeza rushwa.
4

No comments:

Post a Comment